Upo kwa ajili ya Mungu, au Kwa ajili ya Ulimwengu?

Mafundisho October 4, 2023

“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

Warumi 12:1-2.

Mungu anatamani kuona wale wanaodai kuwa wakristo wakiishi kulingana na viwango vya utauwa, jambo la kushtusha ni kuwa pamoja na kudai kwamba tu wakristo bado wengi wetu wamekua wakitaka kuishi katika viwango vya ulimwengu. Baadhi ya wanaume na wanawake wanaodai kuwa wachamungu hawamweki Mungu mbele yao, huwezi kuwatofautisha na ulimwengu katika upande wa mwonekano(mvuto), tabia na mwenendo.

Mara nyingi Neno la Mungu linapoletwa kwa watu hawa ili kuwaonya na kutaka kuwaelekeza katika ukamilifu, wao huishia kulikemea Neno hilo takatifu. Wengine kwa sababu ya kutaka kutimiza tamaa zao wenyewe, wanataka wao ndio walielekeze Neno la Mungu ili likubaliane na mapenzi na matakwa yao wala siyo mapenzi ya Mungu yawaongoze katika kukataa mapenzi yao.

Tunapokuwa wakristo ni lazima tumwakilishe Mungu vyema kama asemavyo katika maandiko yake; “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu… Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze baba yenu aliye mbinguni.” Mathayo 5:13,16. Hebu na tujiulize; Mavazi tunayovaa, vinywaji tunavyokunywa, mambo yote tunayotenda, vyakula tunavyokula, je, vinamwakilisha Mungu kwa ukamilifu, au vinamwakilisha mkuu wa ulimwengu huu (shetani)?

Maisha yetu mara kwa mara yamekua sehemu ya kuchanganya walimwengu ambao wanafahamu kile tunachokiamini ila hawakioni katika mienendo yetu. Hii ndio sababu kama mkristo ukifanya jambo fulani lilisofaa, majirani zetu wasio wakristo huuliza “hadi na fulani kafanya hivi?”  Maana yake ni namna tunavyoshuhudiwa na watu wanaokuzunguka hakuendani kabisa na utume wetu.

Mtu mmoja alitoa ushuhuda kwamba alikuwa duniani akiona uovu mwingi ukitendeka badaye akaamua kuacha ya dunia akijua kwamba akienda kanisani hatayakuta lakini cha kushangaza aliishia kuimba wimbo unaohusu machafuko ndani ya machafuko (confusion on confusion)

Mkristo ni nuru ya ulimwengu anamulika mahali penye giza, na giza haliwezi kutoa nuru bali nuru ndiyo inatoa mwanga na kumulika gizani.

Ikitokea leo kahaba akaja kanisani atajulikana kuwa ni kahaba na anahitaji msaada wa kuelekezwa ili avikwe vazi la ukristo dhidi ya mavazi machafu, na siyo mkristo ambaye anakuja kama kahaba ndani ya kanisa ilhali tayari ameshakuwa ni mkristo, na changamoto ya haya yote ni kwamba wengi tulibatizwa ubatizo wa maji mengi pasipo kubatizwa na ubatizo wa Roho Mtakatifu ndiyo maana watu wanalazimisha ulimwengu uingie katika maisha yao na mwisho ni kulichafua kanisa. Maridhiano na uovu ni mabaya pindi yanaporuhusiwa aidha na mkristo mmojommoja au kundi la watu ndani ya kanisa kama ilivyokuwa kwa kanisa la Pergamo na Thiatira walivumilia uovu na mwisho kanisa likaharibika na giza la kiroho likatawala kanisani ndiyo yanayojirudia leo.

Na mara nyingi haya yasemwapo mwitikio wake unaotoka kwa waumini ni kwamba “unajifanya mtakatifu” hizi ndizo dhihaka zitokeazo mara watu wanapoambiwa juu ya uovu watendao. Na Mungu alishasema kwamba; “Kwa maana imeandikwa, mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” 1 Petro 1:16.

Msisitizo mwingine umewekwa katika Mambo ya Walawi 11:44,45. Juu ya kuuishi utakatifu. Mungu anakuja kuchukua watakatifu yaani wadhambi walioachana na dhambi na siyo wadhambi wanaondelea kutenda dhambi, la!

Pia ni lazima tufahamu uwepo wa neema ya mungu si kutufanya kuendelea na maovu bali neema ipo ili kutusaidia kuachana na maovu na kutenda yaliyo mapenzi ya Mungu na huo ndiyo utakatifu usemwao. Utakatifu ambao unakuzwa kupitia neema ya Mungu kwa kudumu kutenda mapenzi ya Mungu na ukamilifu wote, kwa mujibu wa Tito 2:11-12.

Akizungumzia hali hii mjumbe wa Bwana, Ellen G White anaandika; “Niliona kwamba tangu malaika wa pili alipotangaza anguko la makanisa, yamekuwa yakiendelea kuharibika zaidi na zaidi. Wana jina tu lakuwa wafuasi wa Kristo, lakini haiwezekani kuwatofautisha na walimwengu. Wachungaji hunukuu Neno la Mungu, lakini wanahubiri mambo laini. Jambo hili haliufanyi moyo wa asili kujisikia kuwa na hatia. Roho na nguvu za ukweli na wokovu wa Kristo ndivyo tu viletavyo chuki kwa moyo wa asili. Katika huduma zao zenye mvuto kwa watu hakuna chochote cha kuamsha hasira ya shetani, wala kumtetemesha mwenye dhambi, au kuufanya moyo na dhamiri vitambue uhakika wa hukumu inayokuja karibuni. Watu waovu kwa ujumla hufurahia mfano wa utauwa lakini bila kuwa na utauwa wa kweli, na hivyo watasaidiana kuunga mkono dini ya namna hiyo.” {Early Writings 273.1}

“Mungu analiita kanisa lake kutofautiana zaidi na ulimwengu katika mavazi yao zaidi ya ulivyodhania. Mungu anaendele kuwaagiza watu wake wakimbie kutoka katika kiburi cha mwonekano, kutoka katika kujipenda nafsi, lakini moja kwa moja unafanya kinyume dhidi ya roho wa mungu katika jambo hili, kwa hiyo unatembea gizani na kujiweka kwenye uwanda wa vita wa adui.” (Maisha Yangu Leo. Uk. 106)

Hivyo mpango wa shetani kuhakikisha kwamba:

  • Hakuna tofauti kati ya wakristo na wamataifa katika tabia za kimaadili.
  • Kuhakikisha wakristo wanakuwa sawa na wamataifa katika kuvaa na kujipamba ili isionekane tofauti kati ya ukristo na upagani.
  • Ni mpango wa shetani kuhakikisha mavazi ya kikahaba yanavaliwa na wakristo ili ukahaba uonekane ni jambo la kawaida tu.
  • Ni mpango wa shetani kusiwe na tofauti ya ndoa za wakristo na wamataifa. Ili kuficha nuru ya ndoa inayomwinua kristo.
  • Ni mpango wa shetani kuruhusu nyimbo zisizo za ibada ziendelee kuimbwa huku muziki na falsafa ya muziki wa kanisa ukitupiliwa mbali kwamba ni wa kizamani hauna mvuto na amshaamsha mawazoni mwa wasikilizaji au washikri. Hivyo zinatikiwa nyimbo za kuamshaamsha ambazo hupelelea kucheza na kunengua ambapo nyimbo hizo mkuu wake ni shetani.
  • Ni mpango wa shetani wakristo wasione uzito wa sheria takatifu ya Mungu ili wafanane na ulimwengu.

Haya yote yanafanywa na yanazidi kufanywa na kiwango cha Biblia kikiangushwa chini. Mungu anasemaje katika haya yote?

“Kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza… Na kama walivyokataa kuwa na mungu katika fahamu zao, mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.” Warumi 1:21,28

Saa ingalipo Mungu atusaidie kila mmoja tuweze kuishi kwa viwango vya kikristo na siyo vya ulimwengu huu, kumbuka shetani ana raha za muda kitambo tu, lakini Mungu ana ahadi ya uzima wa milele kwa wote waishio kwa utauwa wakimcha Mungu kwa ukamilifu.


Somo hili limeandaliwa na Mch. Chironge Hezron. Mchungaji Chironge Hezron ni miongoni wa watumishi katika South Nyanza Conference akihudumu katika Mtaa wa Majengo katika mji mdogo wa Nkololo Mkoani Simiyu. Kwa masomo zaidi kutoka kwake fuatilia ukurasa wake wa Facebook

Mch. Chironge Hezron

MCHUNGAJI WA MTAA – MAJENGO, NKOLOLO.

    3 comments

  • | October 4, 2023 at 12:48 pm

    Thanks so much for the powerful and wonderful message 🤝🤝

  • | October 4, 2023 at 1:21 pm

    Amina, Tunabarikiwa na Jumbe hizu

  • | October 24, 2024 at 2:29 pm

    Tunabarikiwa mtumishi

Leave a Reply to Deogratias Kibendela Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *