Siku ya Pili: Kuweka Wakfu na Ukumbusho

Kurejea Madhabahuni – Sehemu ya Kukumbuka

Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.

Mwanzo 12:7

Kuweka Wakfu na Ukumbusho

Katika Biblia, madhabahu daima huwakilisha sehemu za kuweka wakfu na ukumbusho. Ni ishara ya nje ya uhusiano binafsi wa mtu na Mungu, ishara ya ukubali wa mtu na kumwabudu Mungu wa kweli na aliye hai. Madhabahu mara nyingi zilijengwa ili kufanya ukumbusho wa kukutana na Mungu, ukumbusho ulikokuwa na matokeo makubwa katika maisha ya mtu. Mungu alipofanya kitu “kisicho cha kawaida,” “kisicho cha kibinadamu,” au “cha pekee sana,” wapokeaji wa kitendo kikuu cha Mungu hawakutaka kusahau, hivyo wangejenga madhabahu – sehemu ya kukumbuka – katika eneo walipomuona Mungu akitenda.
Mungu alipomwambia Abramu katika Mwanzo 12:7 kwamba angewapatia wazao wake nchi ya Kaanani, Abramu alijenga madhabahu pale kwa sababu namna waliyokutana na Mungu haikuwa ya “kwa kawaida.” Wakati ule Mungu aliahidi kutenda kwa namna isiyo ya kawaida katika maisha ya Abramu na kutoa katika uzao wake taifa kubwa na lenye nguvu. “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako” (Mwanzo 26:24). Isaka alifanya kumbukizi ya mkutano huu wa kimbingu kwa kujenga madhabahu katika sehemu ile ile kwa sababu yeye pia alikutana na Mungu kwa namna “isiyokuwa ya kibinadamu.” Mungu alikuwa amevuka kaida ya asili katika maisha ya Isaka ili kuthibitisha kwamba ahadi yake kwa baba yake Isaka sasa ilikuwa ni ahadi ya Isaka pia. Yakobo, kijana wa Isaka, alisafiri kwenda mahali palipoitwa Betheli (Mwanzo 35:3) na akajenga madhabahu kwa kumheshimu Mungu, aliyemtokea wakati akimkimbia Esau. Kwa sababu kukutana kule na Mungu kulikuwa “kwa pekee sana,” Yakobo alijenga madhabahu pale. Gideoni mwenye hofu alishangazwa sana Mungu alipomtokea kwa Amani na kumuita kuongoza taifa katika ushindi. Gideoni aliguswa sana kiasi cha kujenga madhabahu katika sehemu ile na kuiita “Jehova ni Amani” (Waamuzi 6:24) kwa sababu kukutana kwake na Mungu kulikuwa kwa “Amani sana!’

Kamwe Usisahau

Pamoja na kwamba wengi huona matendo makuu ya Mungu katika maisha yao kama nyakati tu za bahati, wengine hutambua kutenda kwa Mungu na hufanya yote yaliyo katika uwezo wao ili kamwe wasisahau kile alichofanya. Kuna faida ya ziada pia kwa jitihada zao: wasafiri wa siku za usoni katika safari ya maisha wanabarikiwa kwa madhabahu zilizotengenezwa na waamini. Ellen White anaandika kwamba, “Ibrahimu alitupatia mfano wa thamani. Alikuwa ni maisha ya maombi. Popote alipoweka hema yake, aliweka pia madhabahu karibu yake, akiwaita wote katika kambi yake kwa kafara za asubuhi na jioni. Hema yake ilipoondolewa, madhabahu ilibaki. Wakaanani waliokuwa wakizurura walipokea maagizo kutoka kwa Ibrahimu, na wakati wowote mmoja wao alipokutana na madhabahu ile, alimwabudu Mungu aliye hai pale” (Fron Eternity Past, uk. 76).
Ni mibaraka gani ya kimbingu unataka kuikumbuka siku za usoni? Na ni madhabahu gani utamjengea Mungu leo?
Tuzungumze na Mungu wetu.

Wakati wa Maombi (Dakika 30-45)

Kuomba Kupitia katika Neno la Mungu – Mwanzo 12:7
“…Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.”


“Alijenga Madhabahu”
Mungu, siku hii ya leo ninataka kukumbuka kile ulichotenda katika maisha yangu, jinsi ulivyoingilia kati nilipokuwa katika njia isiyo sahihi, jinsi ulivyoniokoa. Ninataka kukumbuka na kukusifu kwa neema yako ya upendo kwangu. Ninakumbuka wema wako, na kama muitikio kwa hilo nitatoa (upya) maisha yangu kwako. Amina.


“Kwa Bwana”
Bwana Mungu, Wewe pekee ndiye unayestahili sifa zetu, ibada zetu, na kujitoa kwetu. Hakuna Mungu mwingine kama Wewe: mwenye upendo mwingi sana, wema mwingi sana, uvumilivu mwingi sana, rehema nyingi sana, nguvu nyingi sana, na aliye tayari kuokoa na kusaidia.


“Watakuwa Watu Wangu”
Mungu, akili zetu zinastaajabu kwamba unaweza kudai sisi ni wako baada ya sisi kukuacha. Asante kwa kutufunika kwa maisha makamilifu ya Yesu Kristo na kutupatia jina jipya (Ufunuo 2:17). Amina.

Mapendekezo zaidi ya Maombi

Shukurani na Sifa: Shukuru kwa mibaraka mahususi na msifu Mungu kwa wema wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na msifu Mungu kwa msamaha wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya eneo mahalia: Ombea mahitaji ya washiriki wa kanisa, familia, na majirani.
Sikiliza na Itika: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa au wimbo.

Mapendekezo ya Nyimbo

  • Saa Heri ya Maombi (#135)
  • Hivi Nilivyo Nitwae (#140)
  • Yesu Kwetu ni Rafiki (#130)
  • Karibu Sana (#33)

    3 comments

  • | January 12, 2023 at 3:49 am

    Asante Kwa masomo mazuri namna hii tunabarikiwa Sana Kwa namna mnavyozama kuyafafanua

    • | January 12, 2023 at 4:02 am

      Amina na karibu tena.

      • | January 12, 2023 at 4:02 am

        Amina, ubarikiwe pia.

Leave a Reply to admin Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *