Siku ya Kwanza - Uko Wapi?

Kurejea Madhabahuni – Kuomba kwa Ajili ya Moyo Uliounganishwa Upya

Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?

Mwanzo 3:9

Swali Muhimu Zaidi

Je, kuna swali la kutafuta zaidi kuliko lile ambalo Mungu alimuuliza moja kwa moja Adamu baada ya kuanguka? Ni kweli, Mungu alifahamu kwa hakika mahali Adamu na Hawa walipokuwa. Hata hivyo, Yeye ni mwenye maarifa – anajua yote, hivyo Mungu hasa alikuwa akimuuliza, Adamu, je, unafahamu ulipo? Adamu na Hawa walikuwa wameacha kumtii Mungu (Mwanzo 3, 4), na kukosa utii kwao kulitengeneza ufa, ufa katika kile ambacho mwanzo kilikuwa ni uhusiano mkamilifu kati ya Mungu na uumbaji wake. Sehemu ambapo Mungu alikuwa akikutana nao siku zote zilizopita ilikuwa tupu siku hii. Sura za kwanza kuwahi kuumbwa, siku ile hazikuwa na tabasamu kwa Muumbaji wao. Mikono aliyoitengeneza kutoka katika udongo haikumkumbatia siku ile. Mioyo ambayo kudunda kwake mara nyingi kuliwiana na moyo wake ilikuwa mbali kwa namna ya ajabu, karibia kuwa kimya kabisa siku ile.

Haitoshi

Ellen White anasema, ”Shetani aliwasilisha kwa wanandoa wale watakatifu dhana ya kwamba wangenufaika kwa kuvunja sheria ya Mungu. Je, hatusikii mawazo yanayofanana na haya leo?” (Patriachs and Prophets, uk. 54). Adamu na Hawa walifanya kosa la kumsikiliza shetani, na aliwashawishi kwamba kile Mungu alichowapatia hakikuwa kinatosha, kwamba ushirika na Mungu katika uhusiano wa karibu, na wenye kuaminiana haukutosha. Ghafla nchi tulivu ya Eden sasa “ilionekana kuwaogopesha wale wanandoa wenye hatia. Upendo na Amani iliyokuwa yao ilikuwa imetoweka, na badala yake walipata hisia za dhambi, hofu ya wakati ujao, utupu wa nafsi. Vazi la nuru lililokuwa limewafunika lilitoweka, na ili kuziba nafasi yake walijaribu kujitengenezea cha kujifunikia; kwani katika hali ile ya kuwa uchi, wasingeweza kukutana na jicho la Mungu na malaika watakatifu” (uk. 57). Dhambi ilikuwa imebadilisha hali ya kiroho ya viumbe pekee katika Eden ambao Mungu alikuwa ameshiriki nao mfano wake halisi. Kwa hakika, iliharibu sura ya Mungu ndani yao.

Muda wa Kuomba

Tangu Adamu na Hawa walipovunja uhusiano wao na Mungu, hadi wingi wa mahusiano ya sasa tunayoshuhudia yaliyovunjika, yamechorwa katika nyuso za watu ulimwenguni, pengine hakuna kingine cha muhimu zaidi cha kuombea kuliko kurejea mahali pale Mungu anapotusubiria. Milenia zinaweza kuwa zimepita, lakini udanganyifu uliomwangusha Adamu na Hawa haujabadilika. Shetani bado anadai kwamba kuna kitu Mungu anatuficha, kwamba Mungu hawezi kuaminiwa, kwamba Mungu hatoshi. Ujumbe huu unatawala zaidi katika kizazi cha kidijitali kilichojikita katika teknolojia, ambapo vifaa vingi na muunganiko mwingi huahidi aina ya furaha ya kiroho, hali ya juu zaidi ambapo sisi wenyewe tunaongoza hatima yetu badala ya kumsujudia Mungu aliyetuumba. Huu ndio wakati wa kukataa udanganyifu wa Shetani na kurejea kwa Yule anayetupenda kwa upendo wa milele, kurudi kwa Yule anayetuvuta kwake kwa Kamba za upendo (Yeremia 31:3)!
Tuombe pamoja…

Wakati wa Maombi (30-45)

Ahadi Yenye Nguvu
“Ni jambo zuri kwamba tunaweza kuomba na kupata tunachokiomba; kwamba viumbe wasiostahili, waliopotoka wana nguvu ya kuwasilisha mahitaji yao kwa Mungu, ni nguvu gani ya juu zaidi mwanadamu angeweza kuitamani kuliko hii – kuunganishwa na Mungu wa milele? Mwanadamu dhaifu, mwenye dhambi ana fursa ya kuzungumza na Muumba wake. Tunaweza kutamka maneno yanayofika katika kiti cha enzi cha Mtawala wa ulimwengu. Tunaweza kuzungumza na Yesu kadiri tunavyotembea njiani, naye anasema, Mimi ni mkono wako wa kuume” (Ellen G. White, Prayer, uk. 7)
Vikundi vyote vya maombi vina namna tofauti ya kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja kwa namna yoyote ile ambayo Roho Mtakatifu ataongoza. Hapa chini pana mfano wa jinsi ya kuomba kupitia kwa Maandiko. Unaweza kuomba kupitia katika aya nyingine za Maandiko pia. Tazama Mwongozo wa Kiongozi kwa ajili ya mawazo mengine ya maombi.

Kuomba Kupitia katika Neno la Mungu – Yeremia 24:7

“Nami nitawapa moyo, wanijue ya kuwa mimi ni Bwana; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; kwa maana watanirudia kwa moyo wao wote.”


“Nitakuwa Mungu wao”
Mungu, asante kwa kuja kututafuta wakati sisi tumefanya mambo yaliyoharibu uhusiano wetu na wewe. Asante kwa kutupenda kwa upendo unaodumu milele na kwa kutuvuta kwako kila mara, na kwa namna ya waziwazi kila dakika ya kila siku. Asante, Mungu, kwa upendo ambao bado huwatafuta wenye dhambi! Amina.


“Kwa Mioyo Yao Yote”
Mpendwa Yesu, tunakushukuru kwa ahadi ya moyo ulioumbwa upya, moyo unaomtafuta Mungu na kumsubiri katika nyakati za uhitaji na nyakati za kujawa. Tunakuomba utimize ahadi yako ya moyo mpya wenye upendo mpya kwako. Amina.

“Watakuwa Watu Wangu”
Mungu, akili zetu zinastaajabu kwamba unaweza kudai kuwa sisi ni wako baada ya sisi kukuacha. Asante kwa kutufunika kwa maisha makamilifu ya Yesu Kristo na kutupatia jina jipya (Ufunuo 2:17). Amina.

Mapendekezo zaidi ya Maombi

Shukurani na Sifa: Shukuru kwa mibaraka mahususi na msifu Mungu kwa wema wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na msifu Mungu kwa msamaha wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya eneo mahalia: Ombea mahitaji ya washiriki wa kanisa, familia, na majirani.
Sikiliza na Itika: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa au wimbo.

Mapendekezo ya Nyimbo

  • Saa Heri ya Maombi (#135)
  • Hivi Nilivyo Nitwae (#140)
  • Yesu Kwetu ni Rafiki (#130)
  • Karibu Sana (#33)

    1 comments

  • | January 11, 2023 at 11:27 am

    Bwana awabariki

Leave a Reply to Damian Kagobya Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *