Kupaka Mafuta Wagonjwa: Huduma inayotatanisha wengi.

Miujiza ya uponyaji wa kimwili inayoendelea katika ukristo mambo leo imehusianishwa sana na kile Yakobo alichokisema juu ya kupaka mafuta wagonjwa. Je tuiogope huduma hii na kuitelekeza kama kilio Cha Mariamu? Wachungaji, na Wazee wa makanisa inahuzunisha kiasi Gani tulivyoicha huduma hii kwa kuwa na maswali juu yake kutokana na visa vilivyofuata maombi yetu yaliyo ambatana na huduma hii? Hebu tuitizame huduma hii kwa mujibu wa Biblia.

Mafundisho October 1, 2025

Na Mch. Amos Thobias

Sauti ya Shemasi wangu mpendwa ilisikika huku akilia “SITAIFANYA KAMWE HUDUMA HII TENA” baada ya kushuhudia kifo cha mama yake mpendwa sana aliyeugua kwa muda mrefu. Ilikuwa siku moja nikiwa katika majukumu ya kutembelea washiriki nikiambatana na Mzee wa kanisa, niliongea na mama yake Mariamu akiwa kitandani, akasema, “mchungaji nimechoka, naomba mnipake mafuta!” Niliwaita watoto wote wa mama Mariamu, nikawaeleza kuhusu ombi la mama,kati ya watoto wote ni Mariamu pekee aliyeonekana kulipokea jambo hili la kumpaka mafuta mama yake wengine, walianza kulia baada ya kuona mama yao anasititiza jambo hili lifanyike. Tuliifanya huduma hii kwa maombi na machozi ya watoto wengine waliotuzunguka,baada ya siku chache mama Mariamu alilala usingizi wa mauti ndipo Mariamu alipolia na kujihisi hatia kwa kuwa alikubali kumpaka mafuta mama yake. Hii haikuwa mara ya kwanza kumtembelea mama Mariamu na kuomba naye, lakini hii ndio ilikuwa mara ya mwisho kuomba na mama Mariamu akiwa hai. Mama huyu alilala mara tu baada ya kufanyiwa huduma ya kupakwa mafuta suala ambalo limeleta na limeendelea kuibua maswali mengi katikati ya jamii ya waumini.

Baadhi ya maswali ni kama haya: je maombi ya wakati huu yaliyo ambatana na kupaka mafuta mgonjwa yalikuwa mabaya? au hayakupata kibali machoni pa Bwana? na je, maombi ya wakati uliopita ndio yalikuwa mazuri na yalipata kibali machoni pa Bwana? Nini haswa maana ya kumpaka mgonjwa mafuta? Nani anapaswa kufanya huduma hii? kwanini huduma hii? Na, Je, ni yapi matarajio ya huduma hii? Miujiza ya uponyaji wa kimwili inayoendelea katika ukristo mambo leo imehusianishwa sana na kile Yakobo alichokisema juu ya kupaka mafuta wagonjwa. Je tuiogope huduma hii na kuitelekeza kama kilio Cha Mariamu? Wachungaji, na Wazee wa makanisa inahuzunisha kiasi Gani tulivyoicha huduma hii kwa kuwa na maswali juu yake kutokana na visa vilivyofuata maombi yetu yaliyo ambatana na huduma hii? Hebu tuitizame huduma hii kwa mujibu wa Biblia.

Biblia na huduma ya kupaka mgonjwa mafuta

Katika Agano la Kale, huduma ya kupaka mgonjwa mafuta haionekani moja kwa moja ikifanyika lakini yapo madokezo ya huduma hii ikiwa kama mojawapo ya desturi za kiibada na kitabibu, ambayo pia ilikuwa na maana ya kiroho. Hii haikuwa tu tendo la uponyaji wa kimwili, bali pia lilihusisha kuomba rehema, kuonyesha huruma,kumkabidhi mgonjwa kwa Mungu, na kama Ishara ya Uponyaji na Baraka.[1]katika Isaya 1:6 kuna dokezo la kupaka mafuta mgonjwa mwenye vidonda na majeraha “Tangu wayo wa mguu hata kichwa, hapana mahali pazima; ni vidonda na michubuko, na jeraha zilizofunguliwa; hazikushindiliwa, wala kupalizwa, wala kupakwa mafuta.Katika andiko hili, tunaona kuwa kupaka mafuta kulihusiana na matibabu ya vidonda na matumizi ya kitabibu.katika  kitabu cha Walawi 14 sura hii, kuna mchakato wa utakaso kwa wale waliokuwa na ukoma. Kuhani aliwafanya wapone au watakaswe na sehemu ya ibada hiyo ni pamoja na kupaka mafuta sehemu za ukoma. Uhusiano na huduma ya Kikuhani Katika Agano la Kale, makuhani walihusika na huduma ya kupaka mafuta si tu kwa wagonjwa, bali kwa vitu na watu waliowekwa wakfu kwa ajili ya Mungu (Walawi 8:10-12). Huduma hii iliwakilisha mamlaka ya Mungu na baraka juu ya mtu au kitu. Katika Agano Jipya huduma hii ilionekana ikifanywa na wanafunzi katika marko 6:13 na msisitizo mkuu wa huduma hii umekuwa katika yakobo 5:14 ambapo tunaona mfano wazi:Yakobo 5:14 “Mtu [2][3]ye yote miongoni mwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa, nao wamwombee, wakimpaka mafuta kwa jina la Bwana.” Hii inaonyesha kwamba desturi hii ilitoka Agano la Kale na kuendelea katika maisha ya kikristo kama tendo la imani na uponyaji.

Maandalizi ya safari ya mwisho

Jambo la kwanza huduma ya kupaka mgonjwa mafuta sio Huduma ya maandalizi ya kifo au Huduma ya kuagana na wapendwa wetu kama inavyochukuliwa.Yakobo anasema “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.” Yakobo 5:14 (Biblia Takatifu) kwa mujibu wa Yakobo na neno alilotumia hapa hawezi (ἀσθενής~ asthenḗs) anaepaswa kupakwa mafuta ni mtu yeyote asiyejiweza kimwili au hata yaweza kuwa kiroho, mwenye homa kali,mgonjwa,aliyechoshwa kwa kuugua sana au aliyeishiwa nguvu kwa sababu ya kuugua ila anazo fahamu. Mazingira aliyopo Yakobo na hadhira anayozungumza nayo inaonesha kuwa alikuwa ana Nena na kusanyiko la kikanisa “Mtu wa kwenu… awaite wazee wa kanisa….” Yakobo 5:14(Biblia Takatifu) sio mitume,waombezi,marafiki au mashemasi ila Wazee[4] japo hii haiondoi ukweli kuwa uponyaji si kwa walio kanisani tu bali ni kwa watu wote maana hata Yesu aliponya wote hata walio onekana kuwa ni wa mataifa Marko7:26-30 “Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake.…  ²⁹ Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako” Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka. Hivyo bado Huduma hii yaweza fanyika kwa watu wote wanaoihitaji ikiwa wanayo Imani sahihi juu ya huduma hii[5]

Awaite Wazee…

Mara nyingi Huduma hii ya kupaka mafuta wagonjwa nimeishuhudia ikifanywa wakati mgonjwa anapofikia wakati wa kutokujitambua hapa ndipo utaona ndugu au watoto wanapata mhaho! Nakuita wachungaji au Wazee je ni sahihi? Hasha! Yakobo anasema “Mtu wa kwenu… awaite wazee wa kanisa….” Yakobo 5:14(Biblia Takatifu) Neno Awaite kwa kiyunani (προσκαλεσάσθω~proskalesasthō) yakobo amelitumia likiwa katika hali ya mtu kujitendea mwenyewe kwa faida yake mwenyewe na ametumia hali ya ulazima (middle voice imperative mood) uwepo wa Aorist kama kitenzi Cha neno proskalesasthō kinatupatia tafsiri ya Hali ya tendo kufanyika mara Moja kwa haraka maana kitenzi ita (καλέω~ kaléō) ni telic hivyo vitenzi vya namna hii huonesha hali ya tendo kutendeka mara Moja (once for all)[6] Kwa tafsiri ya muktadha sahihi wa yakobo 5:14 ni mtu asiyeweza ndie anae waita Wazee wa kanisa na sio ndugu au watoto waliopatwa na mhaho! Wanaoita Wazee wakati mpendwa wao akiwa kwenye koma, tendo la kungojea mgonjwa afike kwenye koma ndipo tuite Wazee kwaajili ya huduma, hii yawezekana ikawa ni miongoni mwa sababu ya kwanini wengi wa wanaofanyiwa huduma hii hulala usingizi wa mauti maana wengi husubiriwa wakiwa mandetendete au wakiwa kwenye koma ndipo wafanyiwe huduma jambo ambalo si sahihi.maana huduma hii haipaswi kucheleweshwa kwa namna hiyo Ellen G White alifanya Huduma hii kwa mgonjwa aliye kuwa na homa (slow fever) anasema “….Wakati tu mkutano ulipofungwa, Dada Meade, ambaye alikuwa ameshikwa na homa, alituomba tusali kwa ajili yake. Tuliingia kwenye chumba peke yetu, ndugu Holt, Wheeler, Stowell, James, na sisi wenyewe.  Baada ya kumpaka mafuta tulimwombea, naye aliponywa…. kwa uwezo wa Mungu”[7]

Huduma iongozayo katika toba

Katika uelewa wa wayahudi ugonjwa ulitizamwa kama matokeo ya dhambi, mtizamo ambao Yesu wakati fulani alipingana nao kwa sehemu, Yohana 9 (Biblia Takatifu)¹ Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. ² Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? ³ Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”. pamoja na hoja ya uhusiano wa dhambi na ugonjwa kuwa na mjadala ambao hata Yesu wakati akiponya alionekana kama kuihusianisha dhambi na magonjwa kwa kauli “…akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.” Yohana 5:14 ni ukweli usiopingika kuwa udhaifu wa kiroho au wa kimwili hupelekea kuishi dhambini[8]mfano wa pekee upo katika kisa cha Ayubu alipougua alishawishiwa toka kwa familia yake kutenda dhambi ya kumtukana Mungu wake.

Huduma ya kumpaka mafuta mgonjwa huambatana na ahadi ya msamaha “…. hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.” Yakobo 5:15 (Biblia Takatifu) kwa kutambua madhara ya dhambi na uhusiano wake juu ya magonjwa Yakobo anatoa ahadi ya pekee sana ambayo huambatana na huduma ya kumpaka mafuta mgonjwa,msamaha! Msamaha huambatana na huduma hii pale mgonjwa anapopata nafasi ya kutubu na kuomba kwa dhati, hakika nguvu ya maombi hakuna awezaye kuipima[9] na hivyo mgonjwa kupata amani ndani yake kuikabili kesho yake maana yuko salama na Mungu wake pamoja na kanisa lake[10] Msamaha wa dhambi si kwa ajili ya watu waliokaribu kufariki au wagonjwa walio kwenye koma bali ni kwa wagonjwa waliochoka kwa kuugua naam wasio katika koma maana swali ni je mgonjwa aliyekatika koma aweza kuita Wazee au wachungaji kwaajili yake mwenyewe, kuungama kwa kanisa na kwa Mungu wake?

Wokovu na kuinuliwa

Kusudi la pili la huduma ya kumpaka mafuta mgonjwa ni wokovu, mgonjwa aliye na uhakika na wokovu wake hata kama atakufa au ataishi ni furaha hata mbinguni, je yakobo anatufundisha kungojea wagonjwa wetu wakiwa katika koma ndipo tuwafanyie huduma ya wokovu hasha! Hili halikubaliani kabisa na fundisho lake juu ya Imani yenye matendo maana kwa Yakobo tunaokolewa kwa Imani yenye matendo maana Imani bila matendo imekufa “Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.” Yakobo 2:17 (Biblia Takatifu) “Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.” Yakobo 2:26 (Biblia Takatifu) “Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua…”  Yakobo 5:15 (Biblia Takatifu) vitenzi okoa & inua katika kiyunani (σῴζω~sózó~σώσει~sōsei &ἐγείρω~egeiró~ἐγερεῖ~egerei) kuwa katika wakati ujao vinatoa wazo kuwa wokovu na kuinuliwa kwa mgonjwa aliyepakwa mafuta hauna msingi wa vitendo kutoke papo kwa hapo au wakati uliopo ila katika wakati ujao licha ya kuwapo kwa mazingira ya vitenzi vya kiyunani vinavyoonekana kaongelea tendo la wakati ujao linalofanyika sasa au limetimia Wakati uliopita na lenye matokeo au madhara ya wakati ujao ( Progressive future tense) hivyo basi jambo pekee linalopaswa kutuvuta kwa huduma hii ni wokovu na kuinuliwa tunakokungojea ajapo mwokozi wetu licha ya kutokutilia shaka kuwa wokovu na kuinuliwa toka kitandani ni hakika maana  kitenzi okoa & inua pia limetumika hapa katika hali elekezi(Indicative mood) hali ya uhakika[11]

Maneno ya mwisho

Huduma ya kupaka mafuta mgonjwa licha ya kuwatatanisha wengi na kuchukuliwa kama huduma yenye lengo la kuagana na wapendwa wetu wakiwa katika koma au huduma ya kuponya kimwili ni huduma ya pekee sana iliyowekwa kando na kuhofiwa na washiriki,wazee isivyobahati hata na wachungaji lakini Yakobo ameiwasilisha kama huduma ya urejeshwaji kama ilivyooneshwa kuhusika na wokovu, msamaha na tukio la ufufuo wa wakati ujao[12]Washiriki,wazee, na wachungaji Kama wanafunzi wa Yesu walivyoitumia huduma hii kwaajili ya injili Marko 6 (Biblia Takatifu)¹²Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. ¹³ Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza” hebu tuitumie kama mkono wa msaada katika utume wa kurejesha sura ya Mungu iliyopotea kwa wanadamu wala tusiiogope.


[1]https://www.google.com/search q=anointing+of+the+sick+in+old+testament&oq=anointing+of+the+sickin+old+&gs_lcrp=egzjahjvbwuqcagbeaayfhgemgyiabbfgdkycagbeaayfhgemg0iahaagiydgiaegiofmg0iaxaagiydgiaegiofmgcibbahgi8cmgcibrahgi8c0gejmzqzmzbqmgo3qaiusaib8qwfvnwi_f69sg&client=tablet-unknown&sourceid=chrome-mobile&ie=utf-8 accessed on saturday september 20/2025 at 18:08pm
[2] Alexander Strauch, Biblical Eldership, p. 284. See pp. 284-91
[3] Kim Papaioannou,anointing the sick:revisting a misunderstood service;ministry international journal for pastors pg8
[4] Strauch, A. (1995). Biblical eldership: An urgent call to restore biblical church leadership. Littleton, CO: Lewis & Roth Publishers.p284
[5]Papaioannou, K. (2016). Anointing the sick: Revisiting a misunderstood service. Ministry: International Journal for Pastors, 88(2), 8–10.
[6] University of Arusha. (2021). Intermediate Greek class notes: Tense & aspect (Chap. 7). University of Arusha.
[7] White, E. G. (1995). Pastoral ministry. Silver Spring, MD: General Conference Ministerial Association.p234.1
[8] Koch, K. E. (1962). Between Christ and Satan. Grand Rapids, MI: Kregel Publications.p183
[9] Durken, D. (Ed.). (2008). New Collegeville Bible commentary: New Testament. Collegeville, MN: Liturgical Press.p782
[10] Ibid pg8
[11] Wallace, D. B. (1996). Greek grammar beyond the basics: An exegetical syntax of the New Testament. Grand Rapids, MI: Zondervan.p448
[12] Ibid pg9

Mch. Amos Thobias ni mmoja kati ya wachungaji wa South Nyanza Conference akihudumu katika Mtaa wa Capripoint Jijini Mwanza.

    12 comments

  • | October 1, 2025 at 8:07 pm

    Nimebarikiwa sana na hili somo kiwastani limenitia moyo na nipende tu kusema kwamba kama Mungu aishivyo azidi kuwatumia watumishi wake kutufunulia maandiko zaidi na zaidi ili pale tunapoelewa na kuwa na tafakari yakinifu katika maisha yetu basi tufanye machaguo ya kuilejea injili na utume wake kristo alio tuachia kwa imani na ujasiri
    Ila nina Swali naomba kusaidiwa na swali langu liko hivi ” Mbali na huduma hii kufanyika kwa wagonjwa je inaweza fanyika kwa mtu ambaye pengine anajiona ana mzigo mzito wa dhambi unao mlemea maishani mwake kiasi kwamba ameshaomba toba na kufanya maungamo lakini bado anajihisi kubwa na hatia je huduma hii anaweza ipata akawaita wachungaji/wazee wa kanisa na mashemasi akaombewa na kupakwa mafuta au ni kwa wale ambao hawawezi tu kiafya au kimwili na si kiroho?? Naombeni kusaidiwa kwa hili

    • | October 3, 2025 at 8:11 am

      Mpendwa Mzigaba ahsante kutuandikia kwakuwa hatuna ushahidi wa kimaandiko juu ya kufanya huduma hii kwa mtu asiye mgonjwa ila anamzigo wa dhambi ahadi tuliyonayo ni hii “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote”.1 Yohana 1:9 (Biblia Takatifu) wito wa kristo kuungama na kwa Imani tunasâmehewa
      Hakuna dhambi nzito ipitayo msamaha wa Bwana Isaya 1:18 inatupa ujasiri, huhitaji kupakwa mafuta ndipo Usamehewe tubu tu utasamehewa.

  • | October 2, 2025 at 2:33 am

    Blessings 🙏

    • | October 3, 2025 at 8:11 am

      Welcome

  • | October 2, 2025 at 4:42 am

    Dunia unahitaji watu Wasomao maandiko na Kuyachambua katika Kina chake, Si watu wa Kukariri wala kusubiria Matamko. Asante Mchungaji kwa Ufafanuzi wa kina, Hakika Uberoya ni sifa Njema.

    • | October 3, 2025 at 8:12 am

      Barikiwa sana Magashi

  • | October 2, 2025 at 7:21 am

    I am very interested with that Biblical lesson. Thanks and May God bless you

    • | October 3, 2025 at 8:18 am

      Welcome brother Kerono 🤗 and thank you for your time with us

  • | October 2, 2025 at 5:24 pm

    Good news

    • | October 3, 2025 at 8:13 am

      Amen, welcome 🤝

  • | October 3, 2025 at 4:14 am

    Ubarikiwe sana Pastor Amos. Umejibu kwa maandiko swali ambalo linaleta wogo wa kufanya huduma hii ya Muhimu kwa kisingizio cha wenzetu wa imani nyingine kuitumia vibaya. Sisi watu wa kitabu(waadventista ndo wanaotakiwa kuitumia kama ilivyoelezwa ktk Biblia) Keep it up Pastor!

    • | October 3, 2025 at 8:16 am

      Thank you Pastor Soka for your lovely comment, welcome 🤗

Leave a Reply to Phinias Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *