Chukizo la Uharibifu Huenda Sambamba na Hukumu ya Upelelezi

Watu wengi wanaofuatilia kutimia kwa unabii, hutumia muda mrefu na kwa makini kufuatilia jinsi unabii wa Ufunuo 13:11-18 unavyotimia haraka. Wafuatiliaji wa karibu wa matukio,hupenda kuonyesha na picha za ushahidi wa viasharia. Hili ni jambo zuri lakini halitakiwi liwe ndilo kipaumbele chetu. Kwa nini?

Baada ya unabii wa siku 2,300 wa Daniel 8:13,14, kumalizika mwaka 1844, kilichoanza na kinachoendelea mbinguni ni Hukumu ya upepelezi. Inaendelea hadi sasa. Sambamba na Hukumu ya upepelezi inayoendelea mbinguni, duniani watumishi waaminifu wa Mungu wanatakiwa kujishughulisha na ujumbe wa utume wa Malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12. Ili wafaulu kuifanya huduma hii inabidi wahakikishe kuwa wanawezeshwa na nguvu za Roho Mtakatifu. Kwa lugha nyingine, wanamvaa Yesu Kristo, wakijiepusha kuuangalia mwili,ili wasiwashe tamaa zake,kwa mujibu wa Warumi 13:11-14. Huduma hii ya kumvaa Kristo inahitaji ubatizo wa kila siku wa Roho Mtakatifu, ambaye huwafunulia kuyajua ayafanuayo mnyama wa Ufunuo 13:11-18. Ni huyu Roho ndiye huwawezesha kuupeleka ujumbe kwa waliotishwa na kutekwa na mnyama, wakiwakumbusha kumcha Mungu na kumtukuza maana saa ya hukumu yake imekuja, (Ufun 14:6,7). Hukumu ya upepelezi inapoendelea mbinguni, duniani ni jukumu la kila mtu binafsi tukajitathmini kuwa Roho amemkumbusha asahihishe nini katika mwenendo wake wa kikristo, kabla ya kufungwa kwa mlango wa rehema, iwe ni kwa kifo cha ghafla au iwe ni kwa uzee.  Kwa nini tunaongelea utendaji wa Papa kwa muda mrefu, badala ya kuongelea dosari za tabia zetu? Tukielewa vizuri anachoenda kufanya Papa mwaka kesho,kitabadilishaje mwenendo wetu? Hivi Kristo alituachia utume wa kumtangaza Yeye kuwa ndiye mwenye kuabudiwa na kutukuzwa na watu wote, au alitupa jukumu la kutangaza vitisho na mateso ya chukizo la uharibifu litekelezwalo na Papa?  Kwa nini tunaonekana kumwinua sana Papa, badala ya kumwinua sana Yesu?  Utendaji wa Papa umekusudiwa kutuonyesha  tulipo kwa mujibu wa Kalenda ya unabii  wa Mungu kabla ya marejeo ya Kristo, pamoja na tahadhali tutakiwazo kuchukua. Kwa nini tunaweka msisitizo kusiko kwenyewe?! Hili likieleweka tutapunguza kutumia muda mwingi kuwajadili wenzetu. Kinyume chake tutatumia muda mwingi kumngangania Mungu kwa kauli kuwa,” SIKUACHI MPAKA UMENIBARIKI”. Hata tukilazimika kuwazia kuhusu mateso yaliyo mbele yetu, bado Mungu atatukumbusha kuwa analiongoza kanisa lake na hatimaye litashinda baada ya kujeruhiwa na yule mwovu, kwa ruhusa ya Mungu. Tukilijua hili ni muhimu tunashughulikia uamsho na matengenezo ya kiroho, katika kutengeneza palipoharibika katika mahusiano yetu na Mungu, badala ya kutumia muda mrefu kujadili mipango ya Papa ya kuwatesa watu wa Mungu. Hii ni kwa sababu mateso hayo Roho atatufunulia tu na kutuandaa.  Tusisahau kuwa mitume hawakuanza utume wao hadi walipopokea uwezo kutoka juu. Sisi pia tuhakikishe tunapokea ubatizo wa Roho Mtakatifu kila siku utakaotuwezesha kumtetea Yesu katikati ya dhoruba.  Kwa mujibu wa Math 22:5 kinachosababisha tushindwe kumtetea Yesu ni udhuru tunaotoa kwa mawakala wa Yesu wanaotualika kwenda arusini. Udhuru ulisema, “Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake, nao waliosalia wakawakata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.”. Tukijiingiza katika kuwapuuzia na hata kuwaua watumwa waliotumwa kutuepusha na ghadhabu ya Mungu, tutajitengenezea hukumu mbaya mwishoni. Mwenye masikio na asikie na kuzingatia.

(Muhtasari umefanywa na Mch Kasika, Mshauri wa Vijana na Wazazi na Viongozi ,0764 151 346).

    5 comments

  • | March 24, 2023 at 7:25 am

    Ujumbe mzito, hebu Bwana atupatie Roho wake mtakatifu tuimalize kaz.

  • | April 28, 2023 at 5:41 pm

    Mungu atusaidie tushinde

  • | March 16, 2025 at 4:08 am

    Amen kwa ujumbe mzuri tumwinue zaidi kristo,,tupokee ubatizo wa roho mtakatifu Kila siku na tuzitafakari njia zetu

Leave a Reply to William Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *