Wakati wa Ibada Takatifu ya Mwenyezi Mungu.

Ujumbe wa Siku December 7, 2023

Ni wakati ambao Malaika wa Mbinguni hujumuika pamoja na wanadamu kumwabudu Mungu wa Mbinguni. Pamoja na hayo akili zote, mawazo yote ya wanadamu na fikra humwelekea Mungu wa Mbinguni Yeye akiwa ni Muumbaji na sisi tukiwa Viumbe wake.

Muziki na nyimbo mbalimbali zenye Utukufu hupenya masikioni na mioyoni mwetu na hapo nafsi zetu zinainuka na kumwelekea Mungu wa Mbinguni akiwa katika Kiti cha Enzi. Huku mioyo yetu ikibubujikwa na Shukrani za pekee Kwake.

Endapo muziki utakuwa si wa kumtukuza Mungu na ukawa ni wa makelele Malaika wa Mungu hutoweka maana hawakai mahali penye kelele, wao hukaa mahali palipotulia penye utulivu na usikivu.

Mjumbe wa Mungu anaandika hivi; “Uimbaji ni sehemu ya ibada ya Mungu mbinguni, nasi tungejaribu, kwa nyimbo zetu za kumsifu, kukaribia, kadiri iwezekanavyo, ulinganifu wa sauti za waimbaji wa mbinguni. Mazoezi mazuri ya sauti ni jambo lenye maana katika mafundisho, lisingedharauliwa. Kuimba, kama sehemu ya ibada ya dini, ni tendo la ibada sawa na sala. Mtu hana budi kusikia wimbo moyoni kabla ya kuweza kuupatia maneno mazuri ya kuufaa.” Kutayarisha Njia 195.2

Hata wapiga vyombo vya muziki na waalimu wanapaswa kuongozwa na Roho Mtakatifu kuvitumia vyombo vya muziki kwa jinsi inavyopaswa wakijua kuwa anayeabudiwa na kutukuzwa ni Mungu wa Mbinguni na si mwanadamu awaye yote. Hivyo kila aina ya muziki na sauti zinazotoka humo zinapaswa kuungana na sauti za waimbaji pamoja na mioyo ya wasikilizaji kumwabudu na kumrudishia Mungu Utukufu, Sifa na Heshima zote.

Kicho na heshima kinahitajika wakati wa ibada huku vikitawaliwa na uongozi wa Roho Mtakatifu na Neno la Mungu likiwa ndani yetu wakati wote na hii ndiyo kumwabudu Mungu katika Roho na Kweli.

Ibada siyo siku ile ya kuabudu pekee, bali ni mtindo wa maisha yako ya kila siku. Maisha yako yanatakiwa kuwa ibada tu popote uendapo. Toa Maisha yako kwa Yesu kila siku ukimwabudu na kumtukuza Yeye pekee. “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Warumi 12:1.

Bwana anahitaji watu watakaomwabudu kwelikweli siyo wa kumfanyia maigizo. Tangu uimbaji, mwenendo na mtindo wa maisha ya kila siku kama wakristo. Lazima Roho wa Mungu ajae Mioyoni mwetu na kutembea katika Neno lake Kila siku. “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.Yohana 4:23.

Wahubiri, waimbaji, walimu, na waumini wapaswa kutambua kuwa kila jambo lolote linalofanywa lapaswa kufanywa kwa utaratibu na kutambua kuwa ni Mungu pekee anayerudishiwa Utukufu. Unapoimba, au kuhubiri kiishi kwanza na kikuongoe pia wewe ndipo ujumbe huo utaweza kuwaleta wengine kwa Yesu. Ikiwa unafanya ibada na hauhisi uwepo wa Roho Mtakatifu moyoni mwako jitafakari mara mbili, je hiyo ibada ni ya kweli au la! Ibada ya kweli lazima ukutane na Mungu katika maisha yako na si kubaki kama ulivyo. Ikiwa ulikuwa na majonzi basi unapomaliza ibada furaha itawale moyoni mwako. Hii ndiyo ibada. Mungu atubariki tunapoyatafakari haya.


Somo hili limeandaliwa na Mch. Chironge Hezron. Mchungaji Chironge Hezron ni miongoni wa watumishi katika South Nyanza Conference akihudumu katika Mtaa wa Majengo katika mji mdogo wa Nkololo Mkoani Simiyu. Kwa masomo zaidi kutoka kwake fuatilia ukurasa wake wa Facebook

MCH. CHIRONGE HEZRON, MCHUNGAJI WA MTAA – MAJENGO, NKOLOLO.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *