Siku ya Tatu: Asubuhi na Jioni

Kurejea Madhabahuni – Mahadhi ya Maisha

Nao wasimame kila asubuhi kumshukuru na kumsifu Bwana, na jioni vivyo hivyo.

1 Nyakati 23:30

Maisha na Mungu

Sura ya 1 Nyakati 23 hudhihirisha kwamba Mungu aliwaagiza Walawi – wale waliotunza hekalu la kale la Kiyahudi na huduma zake – kusimama katika uwepo wake wakiinua sauti zao katika kushukuru na kumsifu kila asubuhi na jioni. Zoezi hili la ibada chimbuko lake ni katika amri nyingine ambayo Mungu alimpatia Musa alipowaagiza Waisraeli akisema “wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao”(Kutoka 25:8). Mungu aliagiza zaidi kuwa, “Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni” (Kutoka 29:39).

Maisha Katikati

Maisha ya Waisraeli yalikusudiwa waweze kuishi kati ya mambo mawili ya kufanyika kila siku, ambayo ni uzoefu wa misingi ya kiroho. Watu wa Mungu walipaswa kuanza na kumaliza siku yao pamoja naye. Hawakupaswa kamwe kudharau neema yake iokoayo. Walihitaji nguvu ya Mungu iwalinde dhidi ya hatari za nje kadiri walivyosafiri nyikani wakielekea katika Nchi ya Ahadi. Walihitaji kulindwa dhidi ya vishawishi vitokavyo ndani – shauku ya kutumia vigezo vya Kimisri na mambo ya kiroho ya Kimisri na mitazamo ya Kimisri waliyokuwa wamejifunza wakiwa utumwani. Kafara za asubuhi na jioni zilikuwa ni namna ya Mungu ya kujenga mpangilio wa kufuatwa na watu na familia za Kiisraeli, namna ya kuwadumisha katika uhusiano sahihi na Yeye. Hapa kuna namna ambavyo Ellen White anaelezea uzoefu huu mtakatifu, wa dhati na wa kila siku:
“Kadiri makuhani walivyoingia patakatifu kila asubuhi na jioni wakati wa kufukiza, kafara ya kila siku ilikuwa tayari kutolewa kwenye madhabahu katika ua wa ndani. Huu ulikuwa wakati wa shauku kubwa kwa waabudu waliokusanyika katika hekalu. Kabla ya kuingia katika uwepo wa Mungu kupitia utumishi wa makuhani, walipaswa kujihusisha katika kuchunguza mioyo yao kwa dhati na kuungama dhambi. Waliungana katika ombi la kimya, nyuso zao zikielekea katika patakatifu. Hivyo maombi yao yalipanda kwa wingu la uvumba, wakati Imani yao ikishikilia kustahili kwa Mwokozi aliyeahidiwa akibainishwa na kafara ya upatanisho. Saa zilizochaguliwa kwa ajili ya kafara ya asubuhi na jioni zilitambulika kama saa takatifu, na baadaye zilitambulika kama muda uliotengwa kwa ibada katika taifa lote la Kiyahudi. Na nyakati kadhaa baadaye Wayahudi wakiwa wametawanyika kama mateka katika nchi za mbali, bado katika saa zile ziliyotengwa walielekeza nyuso zao Yerusalemu na kuomba kwa Mungu wa Israeli. Kwa desturi hii Wakristo wana mfano wa maombi ya asubuhi na jioni. Wakati Mungu akilaani kaida tupu, zisizo na roho ya ibada, huwatazama kwa shauku kubwa wale wanaompenda, wakisujudu asubuhi na jioni ili kutafuta msamaha kwa dhambi walizotenda na kuwasilisha maombi yao kwa mibaraka inayohitajika.” (Patriachs and Prophets, uk. 353, 354)
Ikiwa maisha yako ya maombi yamepoteza mahadhi yake, mwombe Mungu sasa aweze kufanya upya msimamo wako kwa ibada ya asubuhi na jioni leo. Tuzungumze na Mungu wetu.

Wakati wa Maombi (Dakika 30-45)

Kuomba Kupitia katika Neno la Mungu – 1 Nyakati 23:30
“Nao wasimame kila asubuhi kumshukuru na kumsifu Bwana, na jioni vivyo hivyo.”
“Kila Asubuhi”
Yesu, tunataka kuanza siku zetu pamoja Nawe. Tafadhali tuamshe ili tuweze kufurahia ushirika katika uwepo wako. Tusaidia kufanya hili kuwa tabia ya kila siku na siyo kuharakisha au kuacha. Tusaidie kukufanya kuwa wa kwanza na mtangulizi katika mawazo yetu kila siku. Amina.
“Kumshukuru na Kumsifu Bwana”
Baba, sisi ni wepesi kukuletea mahitaji, malalamiko, matamanio yetu mbalimbali, na nyakati fulani tunasahau kwamba Wewe siyo mashine ya kutolea vitu. Tukumbushe kuhusu vipengele vyote vya tabia yako, mambo yote madogo na makubwa uliyotenda na unayotutendea, ili tuweze kukushukuru na kukusifu kwa ajili ya hayo. Sasa, elekeza fikira zetu zikusifu. Amina.
“Na Jioni Vivyo Hivyo”
Mungu, tunatamani siyo tu kuanza siku na wewe bali pia kuimaliza pamoja na wewe. Kadiri tunavyojielekeza katika saa ulizotupatia, tunaomba utukumbushe nyakati nyingi tulipoona uaminifu wako siku nzima. Hebu tulale tukiwa na sifa vinywani mwetu, kwani wewe ni Mwokozi wetu wa milele. Amina.

Mapendekezo zaidi ya Maombi

Shukurani na Sifa: Shukuru kwa mibaraka mahususi na msifu Mungu kwa wema wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na msifu Mungu kwa msamaha wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya eneo mahalia: Ombea mahitaji ya washiriki wa kanisa, familia, na majirani.
Sikiliza na Itika: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa au wimbo.

Mapendekezo ya Nyimbo

Yote Namtolea Yesu (#122)
Uniongoze Jehova (#156)
Karibu Sana (#33)
Magharibi ni Jua (#92)

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *