Na Mch. Amos Thobias
Makambi ni mikusanyiko maarufu sana katika Kanisa la Waadventista wa Sabato inayopendwa na vijana pamoja na wazee, hiki huwa ni kipindi ambapo waadventista hukutana mahali mahali kwa ajili ya ushirika katika Neno, uimbaji, mafundisho na pengine ushirika katika chakula. Licha ya kuwa ni mikusanyiko makini na pendwa nimeona kuna haja ya kujikumbusha juu ya upekee wake na maana ya makambi kiroho kutokana kuwa kanisa linakua na kuna vizazi inawezekana wasielewe umhimu wa mikutano hii na pengine kuichukulia kama mikutano mingine ya kawaida ya kikanisa.
- Karibu miaka 3500 iliyopita NIKO ambaye NIKO aliwafanyia muujiza mkubwa watu wake kwa kuwakomboa kutoka Misri kama ilivyokuwa ahadi yake aliyoinena kwa Abramu (Mwanzo 15:13-14), sikukuu ya vibanda katika biblia ni moja ya sikukuu kubwa zilizokuwa zikifanyika kila mwaka katika taifa la Israeli baada ya mavuno na ilitiliwa msisitizo mkubwa sana katika vitabu vya torati (Lawi 23:33-44, Kumb 16:12-16, Hesabu 29:12-40)
- Wana wa Israeli pamoja na watu wote waliokuwa malangoni pao kama ilivyoamriwa[1] walikusanyika pamoja kusherehekea sikukuu ya vibanda wakikaa katika vibanda vya muda[2] vilivyotengenezwa kwa majani ya mitende kama kumbukizi ya miaka 40 ya kuzunguka jangwani baada ya kutoka Misri na namna Mungu alivyowapigania na kuwatunza safarini.
- Licha ya kuwa makambi yalifanyika mara tu watu walipokuwa wamekusanya mavuno yao toka mashambani (Kumb 16:13) bado kulikuwa na muda maalumu uliokuwa umewekwa kwa ajili ya kusanyiko la sikukuu ya vibanda nao ulikuwa ni siku saba (Lawi 23:34) zikiongezewa siku ya nane iliyoitwa kusanyiko la makini sana[3] siku kuu hii ilianza tarehe kumi na tano ya mwezi wa saba katika kalenda ya kiebrania. Ilikuwa ni sherehe kubwa iliyotanguliwa na siku kumi za kujinyima na toba siku tano tu baada ya siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ijulikanayo kama siku ya upatanisho ambapo dhambi za taifa la Israeli zilifutwa (Lawi 23:27).
Lengo la Sikukuu za Vibanda kwa Wana wa Israeli
- Kukumbuka uaminifu wa Mungu katika kuwatunza watu wake; katika sikukuu ya vibanda Israeli ilisherehekea miujiza ya Mungu. Walikumbuka namna alivyowalisha kwa mana toka mbinguni, kuwanywesha maji toka mwambani, utunzaji kwa wingu mchana na nguzo ya moto usiku (Kumb 8:3).
- Vibanda viliongea juu ya uharaka na uchakavu wa maisha; kwa kuishi katika vibanda Israeli walikumbushwa kuwa maisha yao hapa duniani ni ya muda tu hivyo walitakiwa kuhesabu siku zao. Ili kujipatia moyo wa uchaji waliimba zaburi ikiwemo ile ya 90 yenye Ubeti usemao “…siku za miaka yetu ni miaka sabini,na ikiwa tuna nguvu miaka themanini;na kiburi chake ni taabu na ubatili,maana cha pita upesi tukatokomea mara…” (Zaburi 90:10).
- Walikumbushwa usawa mbele za Mungu; katika siku kuu ya vibanda Israeli walikumbushwa kuwa thamani ya masikini, Tajiri, mjane, yatima, mtumwa, mgeni na wote waliokuwa malangoni pao mbele za Mungu ni sawa ndio maana wote walipaswa kuhudhuria sikukuu hii bila kubaguliwa, wakiwa kama mmoja[4] na walikula pamoja (Kumb 16:14).
- Israeli waliimba na kufurahi pamoja katika sikukuu ya vibanda; katika sikukuu ya vibanda Israeli walifurahia ukombozi wao ambao Bwana aliwatendea toka Misri na kuwaingiza katika nchi ya ahadi “nawe utafurahi katika sikukuu yako… nawe uwe katika kufurahi kabisa…” (Kumb 16:14-15).
- Usomaji wa torati; katika sikukuu ya vibanda ilikuwa ni kipindi maalumu cha kujikumbusha torati ya Mungu hivyo Israeli walikumbushwa juu ya torati na walipogundua wamepungua walifanya matengenezo “…akasoma katika kitabu cha torati ya Mungu…” (Nehemia 8:18).
Sikukuu za Vibanda kwa Kanisa Leo
- Sikukuu za vibanda kwa kanisa leo zipo kulitizamisha kanisa kwenye furaha ya ukombozi iliyo mbele yetu wakati Mungu atakapofanya masikani (kibanda) yake/chake pamoja na wanadamu. (Ufunuo 21:3).
- Sikukuu za vibanda leo zinapaswa kulivuta kanisa pamoja kwa umoja na kuvunja ubaguzi wa aina yoyote miongoni wa waabudu[4]
- Sikukuu za vibanda leo zinatuita kuinua macho yetu kuelekea kwenye ufalme wa milele wa Mungu wetu na maisha ya umilele yasiyoharibika na hivyo kuona kuwa hapa duniani sisi ni wasafiri na wapitaji[5]
- Kama Israeli wa kiroho sikukuu hizi zinatukumbusha namna Mungu wetu anavyojishughulisha sana na mambo yetu ya kimwili na kiroho leo kama alivyojishughulisha na Israeli ya zamani kwa kuwalisha, kuwanywesha na kuwatunza. Kama kanisa wakati huu tunaitwa kuendelea kumtegemea yeye pekee[6]
- Sikukuu za vibanda leo zinakusudiwa kuwarejesha watu kwenye torati/Neno la Mungu kama ilivyotendeka katika Israeli ya zamani jambo ambalo inawezekana wengi leo wamelisahau maana nyakati nyingi utaona watu wakijaa kwenye mikusanyiko ya makambi wakati kwaya zikiwa zinaimba ila ikifika wakati wa Neno kusomwa/kuhubiriwa huanza kutoweka na kuendelea na mambo mengine binafsi kama kupika, kuoga, kupiga picha na marafiki na wengine kwenda majumbani kwao si sahihi kabisa.
Sikukuu ya vibanda kama ilivyokuwa ikitunzwa na kuenziwa hata katika agano jipya tunaiona iliendelea kuwepo. Yohana 7 inaonesha esu mwenyewe alihudhuria mikutano hii ya makambi napendekeza elimu kuendelea kutolewa juu ya upekee wa mikutano hii kiteolojia na sio kuiacha ionekane kama ni mikutano ya kawaida tu ya kikanisa badala yake ionekane kuwa ni mikutano iliyoagizwa na Bwana Mungu kwa kanisa hata leo.
[1] Torati 16:14 “Nawe utafurahi katika sikuu yako,wewe,na mwanao,na binti yako,na mtumwa wako,na mjakazi wako,na mlawi,na mgeni,na yatima na mjane,aliyefiliwa na mumewe,walio ndani ya malango yako”.
[2] Lawi 23:42-43
[3] Hesabu 29:35 BIBLIA TAKATIFU “Tena siku ya nane mtakuwa na kusanyiko la makini sana;hamtafanya kazi yoyote ya utumishi;”
[4] Zbr 133:1” tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza ndugu wakae pamoja kwa umoja”
[5] Ebrania 13:14 “maana hapa hatuna mji udumuo,bali twautafuta ule ujao”
[6] Lawi 23:42-43 “…wazalia wote wa Israeli watakaa katika vibanda;ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwaketisha wana wa Israeli katika vibanda …”

Mch. Amos Thobias ni mmoja kati ya wachungaji wa South Nyanza Conference akihudumu katika Mtaa wa Capripoint Jijini Mwanza.