Kuambatana Huboresha Mahusiano

Kuambatana ni Nini Hasa?

Kuambatana, kumetajwa kwa mara ya kwanza katika Mwanzo 2:24, kuelezea mahusiano baina ya mume na mke. Neno hili limebeba maana pana katika kuboresha mahusiano, siyo na wenzi wetutu bali na Mungu aliyetuumba. Linatumika kikanuni, lengo likiwa ni kuelezea mambo muhimu ya kuzingatia katika kujenga mahusiano yenye afya miongoni mwa waliokubali kujifunga pamoja iwe ni kindoa, kifamilia au kiimani. Ili kuambatana kueleweke, inabidi tafsiri ya kimatumizi, idhihirishayo kuambatana ieleweke inavyodhihirishwa maishani. Kusudi la mada hii ni kufafanua dhana ya Kuambatana maishani, msisitizo ukiwekwa zaidi katika matumizi ya maneno haya; 1. Fuata, andama; 2: Shikanisa Kitu na Kingine; 3: Fungamano, Ushirikiano.

    Muhimu Kueleweka Mapema

    Ni rahisi kuishi kama mume na mke kwa mwonekano wa nje, lakini ikawa vigumu kufungamana kwa kushindwa kushirikishana kifanyikacho. Yawezekana mke akaonekana kumfuata mume, akitumia utii wa woga, kwa hofu ya kutokutenda alichoagizwa kufanya , ijapokuwa hakielewi kutokana na kutoshirikishana. Changamoto mojawapo ya kukosekana ushirikiano miongoni mwa wanandoa ni kuishi maisha yasiyo na uwazi wa maongezi miongoni mwao. Siyo rahisi kushikamanisha kitu na kingine kama kishikanishaji siyo sahihi. Kukosekana kwa umoja hudhoofisha ushirikiano na hupoteza nguvu ya kujisikia wamoja. Kuna umuhimu wa kurekebisha haya kwa kutumia maagizo sahihi ya kushikamanisha watakiwao kuwa wamoja. Matendo yafanyikapo bila umoja,athari zake huwa ni nyingi, na mara nyingi ngumu kutatua madhara yake. Ili kulielewa haya, ni muhimu kutathmini tunavyoishi na atambulikaye kuwa mwenzi kindoa au mwanafamilia.

    Tujifunze Kwa Matukio Halisi

    1. Adam na Hawa waliopewa jukumu hili la kuambatana kwa mara ya kwanza, hatuelewi kisababishi cha mmojawao kwenda bustanini mwenyewe kisha nyoka akamshawishi kuasi maagizo ya Mungu, (Mwanzo 3:1-6). Haikufunuliwa kuwa Adam alikuwa wapi wakati Hawa akidanganywa. Kwa mujibu wa 1Timo 2:14, twaelezwa kuwa Adam hakudanganywa bali Hawa mwenyewe.
    2. Kama Hawa alienda bustanini peke yake, ni kwa nini aamue kutokumshirikisha mumewe! Hatujui maana halielezwi. Fundisho muhimu kutokana na kosa la Hawa ni kwamba kufanya jambo bila kumshirikisha mwenzi kwaweza kusababisha mabaya. Dhambi iliingia ulimwengu kupitia mtu mmoja,(Mwanzo 3:13,15).
    3. Kukubali ushawishi wa mwenzi usiozingatia maagizo ya ujenzi wa mahusiano baina yao na Mungu, wote huingizwa kwenye kosa hilo moja,(Mwanzo 3: 16-19; Warumi 5:12). Ni muhimu kujiepusha na mwelekeo wa aina hiyo katika kuambatana.
    4. Ayubu ni mfano wa wenzi waliombatana mmojawao akimtanguliza Mungu. Ayubu alidumisha mahusiano ya kuambatana na Mungu, kwa kumweleza wazi mwenzake. Wengi wetu hushindwa kuoanisha haya mawili. Inapobidi kudumisha mahusiano ya kuambatana na Mungu, utofauti wa kuambatana kwa wenzi huonekana ili kuonyesha ni heri kumtii Mungu kuliko wanadamu,(Ayubu 2:1-10).

    Kuambatana Kunapopitia Majaribu

    1. Ijapokuwa Adam hakudanganywa na nyoka kuasi maagizo aliyopewa na Mungu alikubali kutumia ushawishi wa mkewe umsahaulishe maagizo ya Mungu. Ukubali huu ulimgharimu kwa uzoefu wa maisha yake, akifundishwa na viumbe asili na watu wa vizazi vyake. Tafsiri ya kuambatana inatakiwa kufafanuliwa akilini mwetu ba Roho Mtakatifu kuliko kujadili hoja hii kisomi tu.
    2. Ayubu aliposhawishiwa na mkewe kumuasi Mungu, alimkemea kwa kumfananisha na mwanamke mpumbavu, asiye furahia mabaya apewayo na Mungu katika kumfundisha mtumishi wake kuambatana naye,(Ayubu 2:9-10).
    3. Mifano ni mingi ndani ya Biblia inayotufundisha kuoanisha kuambatana na mwenzi, bila kudhoofisha mahusiano yetu na Mungu. Kilicho kikuu ni kwamba, kadri tunavyoishi, Mungu aweza kutupima jinsi tunavyoambatana na wenzi wetu,Yeye akibakia kuwa ni wa kwanza kimahusiano kwa kuwa kila mtu aliyemuumba kwa utukufu wake na hutegemewa auonyeshe huo utukufu, ( Isaya 43:7).
    4. Kuambatana na wenzi wetu kunatakiwa kumpatia Mungu utukufu. Hicho kikikosekana, wanaodhani wanaambatana, machoni pa Mungu huonekana kuwa ni vipofu wenye macho na viziwi wenye masikio,(Isaya 43:8).
      5.Elimu ya kujifunza kujenga mahusiano baina yetu na wenzetu, na baina yetu na Mungu, hutoka kwa Mungu. Mataifa yote hutakiwa kufundishwa kuujua ukweli huu. Ni muhimu kwetu kujizoeza kuishi kama mashahidi wake, aliotuchagua kama matokeo ya kumwamini na kumtegemea kuwa hakuna mwenye uwezo ulinganao na uwezo wa Mungu. Kutii maagizo yake kutatuweka huru hatimaye.
      Imeandaliwa na Mch E. Kasika, Mshauri wa Vijana na Wazazi na Viongozi, +255 764 151 346

      Leave a Comment

      Your email address will not be published. Required fields are marked *