Na Mch. Sam Neves
Kanisa la Waadventista Wasabato limekusudia kusambaza nakala bilioni 1 za kitabu cha Pambano Kuu cha Ellen G. White kote ulimwenguni katika lugha mbalimbali ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024. Waadventista wengi wamefurahi na wanasubiri kwa hamu kununua vitabu hivyo na kuanza kuvigawa. Hata hivyo, wapo wengine wanaoshangaa kuhusu gharama na ufanisi wa mradi huu. Fikiria mambo yafuatayo;
Mradi huu unawakilisha gharama ya kifedha ambayo inaweza kuzidi Dola za Kimarekani Bilioni moja. Pili, washiriki wanahimizwa kusambaza vitabu hivi binafsi jambo linalomaanisha matumizi ya kiasi kisichopimika cha rasilimali yenye thamani kubwa sana — muda. Tatu, mradi huu utaathiri sayari dunia kwa sababu inakadiriwa kuwa zaidi ya miti milioni 8 itakatwa ili kutengeneza karatasi kwa ajili ya kuchapisha vitabu hivyo. Mwisho, wapo pia wanaoamini kuwa mradi huu wa Pambano Kuu unaweza pia kuharibu sifa ya Waadventista Wasabato kwa vile vitabu hivyo vinaweza unaleta ukosoaji kutoka kwa jamii.
Je, bado inafaa kama kanisa kuhamasishana kusambaza nakala hizi bilioni 1 za Pambano Kuu? Je gharama hiyo ni kubwa mno? Je, tunapaswa pia kutathmini kama hiki ndicho kitabu bora zaidi kugawa kwa wakati huu? Je, kuna njia bora Zaidi ya kuwafikia watu kwa gharama nafuu zaidi?
Je, Gharama Ni Kubwa Sana?
Sura chache za mwisho za Biblia zinaeleza habari Yerusalemu Mpya ukishuka kutoka mbinguni kama bibi harusi (Ufu. 20-22). Waliookolewa wako ndani ya jiji hilo, na baada ya Kristo kuvikwa taji, Shetani anaongoza kila mtu aliye nje ya jiji hilo kushambulia jiji kwa mara moja ya mwisho.
Kwa wakati huu nina hakika wengi wetu tunajiona tukiwa ndani ya jiji, tukitazama kwa hofu kile kitakachotokea. Moto unakaribia kuteketeza uovu na wale waliochagua wote kushikamana nao. Hebu fikiria macho yetu yakiona nembo ya Waadventista wa Sabato kwenye moja ya majengo yanayoteketezwa. Kila kitu ambacho tumewahi kukitamka kama cha Waadventista wa Sabato kinakaribia kuteketezwa. Kuna jumba chakavu lililojaa vitabu vya Pambano Kuu, ambavyo bado viko kwenye maboksi yake, havijasambazwa. Macho yetu yanageukia misitu iliyong’olewa ya ulimwengu, ambayo pia inakaribia kuharibiwa. Hatimaye, moto ule mkuu unapoanza kwa ukali, tunakaza macho yetu kwa watu.
Je, hatungetamani sasa, kwa mioyo yetu yote, kwamba miti hiyo ingegeuzwa kuwa vitabu vingi zaidi ili kusomwa na watu wengi zaidi? Labda wengi wao sasa wangekuwa karibu nasi, wakiwa salama na wazima, ndani ya jiji.
Tunapoitazama kupitia lenzi hii, mashaka yetu huonekana kwa namna tofauti. Sifa yetu, kama watu na kama kanisa, ni vya pili ikilinganishwa na kusaidia watu wengi zaidi kuwa salama ndani ya jiji hilo. Vivyo hivyo, pesa zetu na muda wetu pia. Ingawa linaweza kuonekana kuwa jambo utata, licha ya jukumu letu la kutunza sayari yetu, miti pia inakua swala la pili tunaposhughulika na wokovu wa watu.
Hata hivyo, ni juu ya mti ambapo Yesu alihakikisha wokovu wa watu wote. Ikiwa thamani ya ubinadamu inapimwa kwa damu ya Kristo, hakuna kitu kingine kinachopaswa kutuzuia kuwasaidia kuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake, ikiwa ni pamoja na sifa zetu, wakati wetu, fedha zetu, na ndiyo, miti yetu.
Je, Hiki Ndicho Kitabu Bora Zaidi Kusambaza?
Kama Waadventista Wasabato, tumebarikiwa kuwa na wingi wa vitabu tunavyopaswa (na kuweza) kuugawia na ulimwengu; Vitabu juu ya maisha ya afya, maisha ya familia, elimu, uwakili, na zaidi. Maandishi ya Ellen White hasa yanatoa umaizi wa ajabu katika maisha na mafundisho ya Yesu Kristo, ikijumuisha vitabu kama Njia Salama na Tumaini la Vizazi Vyote.
Ingawa hatupaswi kupuuza kugawa vitabu hivi ambavyo vimegusa mioyo ya mamilioni ya watu, tunaishi katika nyakati zisizo za kawaida sana, na watu wanatazamia wakati ujao kwa hofu na kutokuwa na uhakika. Ulimwengu unaonekana kuyumba kutoka katika shida moja hadi nyingine, na watu wanatafuta, wakitamani, majibu ambayo ulimwengu hauwezi kutoa.
Kitabu cha Pambano Kuu kinatoa majibu thabiti ya kibiblia kwa yale ambayo yametokea zamani, yale yanayotokea sasa, na yatakayotokea wakati ujao. Kinafunua pazia katika ulimwengu usioonekana ambapo vita halisi na kubwa sana inaendelea. Kinafichua mipango ya adui na kuelekeza njia ya uzima wa milele. Hii ndiyo sababu Pambano Kuu kilikuwa kitabu ambacho Ellen White alitamani kuona kikisambazwa kwa upana zaidi kuliko vitabu vyake vingine vyovyote.
Je, Tunaweza Kupata Mbinu Zinazofaa Zaidi?
Licha ya fursa nyingi mpya zilizoletwa na kukua kwa teknolojia, kuna angalau sababu tatu muhimu za kutanguliza usambazaji mkubwa wa nakala ngumu ya kitabu cha Pambano Kuu juu ya mbinu mpya za kidijitali.
Udhibiti wa Kidijiti (Digital Censorship); Katika miaka michache iliyopita Kanisa la Waadventista Wasabato limewekeza mamilioni ya dola katika tovuti, majukwaa ya mitandao ya kijamii, na program tumishi ambazo yameweka machapisho yetu ya kidijitali kwa njia ambayo watu wanaweza kuyapata, kuyafuatilia, na kuyapakua. Hili limefanywa kupitia uboreshaji wa injini ya utafutaji, uundaji wa maudhui, uundaji wa program tumishi, na utunzaji wa kichungaji mtandaoni, na kusababisha kila uhusiano wa mtandaoni kugeuzwa kuwa uhusiano wa ana kwa ana. Tunahitaji kuendeleza matumizi ya teknolojia na fursa hizi kwa sababu zinapatikana sasa, lakini hii inaweza isiwe kweli kwa wakati wote. Ikiwa bado tunaamini katika ujumbe wetu ya kinabii, na kwamba ulimwengu utazidi kuwa mahali penye changamoto zaidi kushiriki injili, lazima tutegemee njia nyingine zaidi ya teknolojia za kidigitali ili kumaliza utume wetu. Kwa nini? Kwa sababu ya udhibiti.
Miaka miwili iliyopita imeonyesha, bila shaka, kwamba akaunti zetu za mitandao ya kijamii na programu tumishi zinaweza kuondolewa kwenye majukwaa husika katika kufumba na kufumbua. Tovuti pia ni vilevile. Katika mchana mmoja inawezekana kuondoa kila kitu ambacho kanisa limewahi kuchapisha mtandaoni.
Ni muhimu kwamba tusambaze Pambano Kuu kabla ya matukio haya kutokea, ili kila kaya iweze kupata kitabu nyumbani kwao. Mamilioni ya Waadventista wamejifunza ukweli kwa sababu familia zao zilisoma Pambano Kuu wakati fulani. Mamilioni ya watu wataokolewa kwa sababu ya usambazaji huu mkubwa wa vitabu.
Ushiriki wa Kila Mshiriki; Kuhamasishana kwa pamoja kunaweza kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo, kwani tamaduni zetu ni tofauti sana. Hata hivyo, wengi wetu tunaweza kuchochewa kununua vitabu vichache na kuvisambaza binafsi. Mbinu hii iliyogatuliwa ya kugawa inahimiza ushiriki wa binafsi badala ya kutuma vitabu kwa watu. Muunganiko wa kibinadamu ni muhimu na unaweza kuwa tukio la kuokoa maisha kwa wale wanaopokea vitabu. Kwa kuzingatia kwamba usambazaji wa kidijitali wa Pambano Kuu pia huchangia kufikia lengo, washiriki waliobobea katika ufikiaji wa kidijitali wanahimizwa sana kutumia ujuzi wao kwa njia hii pia. Utumiaji wa mbinu moja haupaswi kutuzuia kutumia njia nyingine pia.
Sababu ya Kiuchumi; Uchapishaji wa wingi wa pamoja na ugatuaji wa usambazaji wa wingi hufanya iwezekanavyo kufikia gharama ya chini kwa kila kitabu. Hili linaweza kufikiwa tu wakati kuna juhudi zilizoratibiwa kwa muda mfupi na watu wengi.
Je, Ukweli wa Sasa ni Jambo Lililopitwa na Wakati?
Msingi mkuu wa mradi huu wa usambazaji wa Pambano Kuu ni imani kwamba Kanisa la Waadventista Wasabato ndilo kanisa la masalio la unabii wa Biblia, lililopewa jukumu la kutangaza injili ya milele kabla ya ujio wa pili wa Kristo. Tunaamini kwamba Mungu ametupa utume kwanza, na kisha muundo wetu, rasilimali, huduma, na mali zetu zote, ambazo zipo ili kutimiza utume huu.
Katika historia ya vuguvugu hili tumewasihi wapendwa na majirani, pamoja na wageni, walio karibu na walio mbali, wajitayarishe kwa siku ile tukufu na ya kutisha wakati mbingu itakapofunguka na Yesu atarudi. Katika miaka ya hivi majuzi, hata hivyo, kumekuwa na hisia zinazoongezeka miongoni mwa washiriki wetu kwamba kanisa letu ni jumuiya tu kama jumuiya nyingine za kiimani zinazomwamini Yesu. Baadhi ya Waadventista wanaamini kujitambulisha kama masalia ni kiburi na majivuno, na hivyo kuzuia utume wetu wa kufanya wanafunzi. Wengine wanadai kwamba tunapaswa kuacha kuhubiri maangamizi na huzuni na kuzingatia Injili badala yake. Ukweli wa sasa unapaswa kusisitiza tu maisha, kifo, na ufufuo wa Yesu. Wanafikiri ulimwengu wetu umegawanyika sana kiasi kwamba tukihubiri ukweli wa sasa kama walivyofanya waanzilishi wetu, tutaonwa kama dhehebu lingine tu linalotawaliwa na nadharia zisizo za maana.
Hoja hizi huonekana kukubaliwa wale ambao wameamini katika hekaya za kanisa lisiloweza kukatalika. Wale ambao wamesadikishwa kwamba tunapounda makanisa ya kukaribisha ambayo yanapunguza mateso ya wengine katika jumuiya zetu, mamilioni watakuwa Waadventista Wasabato kwa uwezo kamili wa wema wetu. Hekaya hizi huharibu uwezo wetu wa kutimiza utume wetu mkuu wa kutangaza ujumbe wa malaika watatu kama ilivyotabiriwa katika Ufunuo 14. Katika historia ya Ukristo hakujawahi kuwa na wakati ambapo masalio waaminifu hawakuteswa au kuidhinishwa.
Tunapaswa, kwa njia zote, kutumia mikakati bora ya kuusambaza na kuuishi utume wetu kwa upendo na huruma. Walakini, ikiwa upendo huu hauonekani katika changamoto ya “kumfuata Yesu” kwa gharama yoyote tunaposhiriki maono ya kinabii ya Mungu na wengine, tunakua hatutimizi utume wetu. Ukweli wa sasa sio jambo lililopitwa na wakati. Tangu wakati wa waanzilishi wetu, mtazamo wetu juu ya ukweli umekua. Tuna ujumbe mzuri zaidi na wa dharura wa kumpa kila mwanadamu. Hebu tuanze kwa kununua nakala za Pambano Kuu ili kugawa kama zawadi kwa wapendwa wetu, majirani, marafiki, wafanyakazi wenzetu, na wageni. Hebu tukusudie kuwasaidia watu wengi kadri tuwezavyo kuingia ndani ya jiji katika siku ile kuu ya hukumu.
Makala hii iliandikwa na Mch. Sam Neves ambae ni Mkurugenzi Mwenza wa Idara ya Mawasiliano ya General Conference na kuchapishwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya kiingereza na tovuti ya Adventist World na imetafsiriwa kwa ruhusa na ofisi ya tehama ya South Nyanza Conference. Waweza kusoma makala halisi katika lugha ya Kiingereza hapa.