Siku ya Saba: Kanisa Linaloabudu

Kurejea Madhabahuni – Hitaji Letu la Muhimu Zaidi

Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.

Zaburi 95:6

Ibada (isiyo) ya Kawaida

Utafiti wa Waadventista wa Sabato wa dunia nzima wa mwaka 2018 uligundua kwamba ni asilimia 34 tu ya nyumba za Kiadventista inayojihusisha katika ibada za kila siku za asubuhi na jioni, na asilimia 52 tu ya washiriki wa kanisa ndio wana ibada yoyote binafsi. Je, kanisa lenye ujumbe wa wakati wa mwisho uliojikita katika ibada (ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12) linaweza kuwasilisha ujumbe huu muhimu ikiwa washiriki wake hawajihusishi kwa uaminifu katika ibada binafsi na za familia? Kwa maneno mengine, tunaweza kutangaza kwa ufasaha kile ambacho wengi wetu hatufanyi kila siku?
Ellen White anasema, “Hakuna kingine zaidi kinachohitajika katika kazi [ya Mungu] kuliko matokeo ya ushirika na Mungu” (Testimonies for the Church, gombo la 6, uk. 47). Sehemu nyingine anaandika kuwa, “Kama wazee wa zamani, wale wanaokiri kumpenda Mungu wanapaswa kujenga madhabahu kwa Bwana popote watakapoweka kambi zao… Baba na Mama wanapaswa mara nyingi kuinua mioyo yao kwa Mungu katika maombi ya unyenyekevu kwa ajili yao na watoto wao. Hebu baba, kama kuhani wa nyumba, aweke katika madhabahu ya Mungu kafara ya asubuhi na jioni, huku mke na watoto wakiungana katika maombi na sifa. Katika nyumba kama hiyo Yesu atapenda kukaa” (Child Guidance, uk. 518, 519)

Hitaji Letu la Muhimu Zaidi

Kurejesha ibada binafsi na za familia kati ya Waadventista wa Sabato pengine ni hitaji kubwa zaidi kuliko yote katika wakati wetu. Lakini haitakuwa rahisi. Leo tunakabiliwa na changamoto ya teknolojia inayotawala muda wetu kwa kasi na kubadili akili zetu. Uraibu wetu kwa vyombo vya habari, hasa mitandao ya kijamii, umetuacha na wasiwasi, na kutufanya kuudhika kirahisi, kujikuta wapweke, wenye msongo, kukosa usingizi, na tusiofurahia hali yetu katika maisha.
Tofauti na hivyo, ibada binafsi na za familia zinakuwa na matokeo yaliyo kinyume. Ibada hutuliza akili zetu, hupunguza upweke, hupunguza msongo, huongeza Amani, hukamilisha mahitaji yetu ya kihisia, na kutufundisha kuridhika. Je, madhabahu inaweza kuwa tiba ya akili zetu zilizochoka na kuvurugikiwa, na mioyo yenye wasiwasi?
Mungu anatuita wakati huu kuliko wakati mwingine wowote, turudi katika moyo wake, tudumishe muda wa kujifurahisha katika uwepo wake. Hii ndiyo sababu kanisa la Waadventista wa Sabato limeanzisha mkakati wa “Kurejea Madhabahuni”, jitihada ya kujenga upya madhabahu binafsi na za familia katika kanisa la Mungu. Kufikia mwaka 2027 tunatamani kuona angalau asilimia 70 ya washiriki wa Kiadventista wanajihusisha katika ibada za binafsi na za familia za asubuhi na jioni. Utasikia zaidi kuhusu mpango huu katika siku zijazo, lakini sote tunaweza kuanza sasa kwa kumwabudu Mungu kwa uaminifu na kwa mpangilio. Ikiwa Tunarejea Madhabahuni pamoja na Mungu, tutabadilishwa na kufanana na mfano wake na kutiwa nguvu kuimaliza kazi yake!
Hebu tumuombe Mungu leo kwa ajili ya kumwagwa kwa Roho Mtakatifu kwa namna maalumu katika uzoefu wetu wa ibada pamoja nae. Wakati huu zaidi, tunahitaji mbaraka wa pekee wa kuwa na ushirika na Mungu.
Tuzungumze na Mungu wetu.

Wakati wa Maombi (Dakika 30-45)


Kuomba Kupitia katika Neno la Mungu – Luka 6:12
“Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.”
“Njoni, Tuabudu na Tusujudu”
Ee Mungu, ni mara nyingi kiasi gani tumeshindwa kutambua jinsi ulivyo mkuu na mwema na unayepita fahamu za wanadamu. Ukubwa wa ulimwengu hauwezi kukufunika, na bado mara nyingi hatukuheshimu au kukuabudu inavyopaswa na kwa heshima kubwa. Tuonyeshe utukufu wako na tusaidie tuweze kutambua jinsi unavyostahili heshima, utukufu, na sifa zote. Tukumbushe tukukaribie kwa heshima na kicho, tukikutambua kama Mungu wetu mkuu. Amina.
“Tupige Magoti Mbele za Bwana Aliyetuumba”
Ee Mungu, Muumba wa vitu vyote, wewe ndiye Mbunifu Mkuu. Vitu vyote ulivyoviumba ni vizuri na vikamilifu. Upendo wako umeandikwa katika kila jani na kila ua linalochanua. Wewe pia ni Baba yetu wa kweli, Uliyetuumba, ukatutamani, na kutufanya kwa mfano wako. Ni kwa namna gani tunaweza kutambua kikamilifu heshima uliyoweka juu yetu ya kuitwa watoto wako? Tunakusifu na kukuabudu, Muumbaji wetu! Amina.

Mapendekezo zaidi ya Maombi

Shukurani na Sifa: Shukuru kwa mibaraka mahususi na msifu Mungu kwa wema wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na msifu Mungu kwa msamaha wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya eneo mahalia: Ombea mahitaji ya washiriki wa kanisa, familia, na majirani.
Sikiliza na Itika: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa au wimbo.

Mapendekezo ya Nyimbo

Nina Haja Nawe (#126)
Na Tumwabudu (#5)
Yesu Uje Kwetu (#13)
Yanipasa Kuwa naye (#154)

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *