Matendo ya Mwili Huathiri Mahusiano

Mioyo iliyovunjika haiwezi kutiwa moyo na nyuso zilizokasirika au na sauti kali isiyo na upole au huruma. Watu wenye mawazo mengi na waliokata tamaa hawasaidiwi kurejesha matumaini na mtu aliye mbali, akidai kuwa anawaombea Mungu awasaidie. Kufariji hudhihirishwa na kujali kwa matendo mema yaonyeshayo huruma. Ni kweli kuwa maombi husaidia, lakini uwepo wa mfariji unaongeza ushahidi wa mwonekano wa kujali. Kukosekana kwa matendo ya aina hii kumechangia sana kukosekana kwa uaminifu katika biashara za marafiki ambao hawakutegemea kuwa wangelidhulumiana katika biashara hizo. Kukosekana kwa lugha zenye kujali na kusikiliza kwa kubadilishana mawazo, kumechangia sana kutokujua kinachoendelea moyoni mwa mwenzi au baina ya mzazi na mtoto. Kumezua mashaka na fikra za kudhania yasiyo kuwepo kwa kuwa hakuna njia rahisi ya kujua yanayoendelea. Je, msomaji unaishi ndani ya familia yenye mahusiano ya aina hii au unaishi katika familia iliyo huru kujadiliana na kutenda kwa wazi kila mmoja akifurahia kuwa sehemu ya familia hiyo?

Wapo wanaopuuzia mwonekano wa matendo ya mwili kwa nje kwa madai kuwa Mungu huangalia moyo. Hoja hiyo ni miongoni mwa hoja dhaifu,kidini na kiroho na kijamii. Haupo moyo unaoweza kuongea ili sauti yake imtie nguvu aliye kata tamaa. Kinachoongea ni mdomo. Mara nyingi vijana huchagua marafiki wa kike kuwa wachumba wao kwa hoja kuwa moyo wake umempenda. Moyo hauwezi kupenda wakati hauoni. Anachosema ni kwamba macho yake yamependezwa naye,yakashawishiwa kumpatia uzuri asiolazimika kuwa nao kitabia au moyoni. Kijana Samson, alipoutamani uzuri wa mwonekano wa yule binti Delila, alimwambia baba yake kuwa,” Ananipendeza sana“, (Waamuzi 13:3). Samson hakujua kuwa huyo binti alikuwa atumiwe kumfanya awe mateka wa Wafilisti kwa kumshawishi kueleza yaliyo siri ya nguvu zake za ajabu, (Waamuzi16: 5-19). Vijana wengi uharibu mahusiano yao kwa kudanganywa na lugha zintekazo akili na mawazo yao ili miili yao itekwe na kutumiwa kama mapambo ya maigizo. Hiki ndicho alichokifanya Samson. Baada ya kutobolewa macho aligeuzwa kuwa ni sanaa ya maonyesho ya kuwachezea michezo Wafilisti katika ukumbi wao, (Waamuzi 16:20-25). Kilichotobolewa hakikuwa moyo bali ni macho. Michezo ya Sanaa haikuchezwa na moyo bali na viungo vyote vya mwili vilivyohusika na michezo hiyo. Haiwezekani kudai kuwa Mungu huangalia moyo kwa ndani bila uhusiano na nje ya mwili.

Yesu Atahukumu Wanadamu Kwa Matendo Waliyotenda Kwa Mwili

Tamko hili limeandikwa katika 2 Wakorintho 5:10. Matendo mazuri yatalipwa ujira nzuri. Matendo mabaya yatalipwa ujira mbaya wa adhabu. Matendo yote yasiyoonyesha huruma,au upole, wala kujali wala kumpendeza Mungu, yanafanywa kumpendeza mwingine aliyechaguliwa kuwa mlengwa aonekanaye kuwa ndiye mamlaka inayokubaliwa. Mungu aliagiaza kuwa mlapo,au mnywapo au mfanyapo neno lolote,fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu, (1Wakor 10:31). Utendaji huu unao ongelewa hapa ni utendaji wa matendo ya mwili,siyo utendaji wa moyoni. Hii ni kwa sababu yaliyo moyoni siku zote hulazimika kuonyeshwa nje ili mtendaji awe nuru ya ulimwengu, watu waone matendo yake wapate kumtukuza Mungu aliye mbinguni, (Math 5:14-16). Ni kwa sababu hii Yesu alisisitiza umuhimu wa matendo ya huruma ya kuwahudumia walio wahitaji, kama tusomavyo katika Mathayo 25:31-44. Aidha katika Ufunuo 21:8, tunaorodheshewa matendo maovu yatakayo sababisha wayatendayo wasiokolewe na Yesu. Orodha hii inahusisha: Waoga, wasioamini, wachawi, wachukizao, waabudu sanamu na waongo wote, kuwa sehemu yao ni katika ziwa la moto.

Mtume Paulo na mtume Petro, wote wakiongelea suala la mapambo, wanaonyesha dhana ya aina moja. “Kujipamba kwenu kusiwe kujipamba kwa nje,yaani kusuka nywele, na kujitia dhahabu,na kuvalia mavazi, bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyo haribika; yaani, roho ya upole na utulivu,iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu“,(1 Petro 3:3,4). Mtume Paulo ameliandika kwa lugha hii,”Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”,(1Timoth 2:9,10).

Hitimisho

Kila anayeukiri uchaji wa Mungu, mwonekano wake wa nje hauwezi kutofautiana na alivyo ndani. Kwa lugha nyingine, nje hueleza ndani ya akili na moyo wake. Wanaopenda kujigeuza waonekane tofauti kutegemeana na mazingira waliyomo kijamii,hao hawaonyeshi uchaji kwa Mungu,bali huonyesha uchaji kwa jamii,iwe ni ya kidini au ya nyingineyo. Hii ndiyo tofauti makusanyiko ya kisherehe huwaonyesha wavaaji na watendaji wengine tofauti na wanavyokuwa katika makusanyiko ya kiibada. Hawa huonyesha kuwa wanayo mionekano ya aina mbili. Wakienda kwenye sherehe huvaa kana kwamba Mungu hayupo na kwamba haoni wakifanyacho. Wakienda katika ibada, huvaa kumridhisha Mungu. Ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu hadhihakiwi, na kwamba apandacho mtu ndicho atakachovuna. Hukumu ya wanadamu wote itaendeshwa na Yesu peke yake,ikilenga kufuatilia matendo ya mwili,ili kila mtu apate ijara ya aliyotenda kwa mwili,kwa uzuri wake kwa Mungu, au kwa ubaya wake. Ni katika uelewa huu,maisha ya kujifanya,au unafiki ni mabaya na yatakuwa na malipo mabaya. Ni muhimu kutafakari matendo ya miili yetu kadri tunavyoishi maana yanafuatiliwa na Mungu kila siku.

(Muhtasari umefanywa na Mch E.Kasika, Mshauri wa Vijana na Wazazi na Viongozi, 0764 151 346).

    2 comments

  • | January 6, 2023 at 10:01 am

    Hakikla ubarikiwe, maana aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Pia kinywa huyanena yaujazayo moyo, tukibadilika ndani na nje tutabadilika.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *